FIGO KUFELI KWA MGONJWA WA KISUKARI

Medikea Clinic

Medikea Clinic

FIGO KUFELI KWA MGONJWA WA KISUKARI

Tangulizi

Kisukari ni hali ya mwili kushindwa kutoa insulini ya kutosha (homoni inayosaidia kudhibiti viwango vya sukari kwenye damu). Sukari ya damu inapokuwa juu huweza kuharibu mishipa ya damu, hivyo mishipa ya damu kushindwa kufanya kazi na kusababisha shinikizo la damu ambalo linaweza kuharibu figo.

Kazi kuu ya figo ni kuchuja taka na maji ya ziada kutoka kwenye damu ili kutengeneza mkojo. Pia husaidia kudhibiti shinikizo la damu na kutengeneza homoni ambazo mwili unahitaji ili kuwa na afya njema. Ugonjwa wa kisukari ndio sababu kuu ya ugonjwa wa figo. Takribani mtu mzima mmoja kati ya watatu wenye ugonjwa wa figo huwa na ugonjwa wa kisukari.

Ugonjwa wa kisukari unaweza kusababisha kufeli kwa figo, ambayo ndiyo hatua ya mwisho ya ugonjwa wa figo. Kushindwa au kufeli kwa figo ni hali inayotishia maisha kwa mgonjwa.

SABABU ZINAZOPELEKEA KUFELI KWA FIGO KWA MGONJWA WA KISUKARI:

  1. Sukari ya juu ya damu isiyodhibitiwa (hyperglycemia).
  2. Shinikizo la damu lisilodhibitiwa (hypertension).
  3. Historia ya familia ya ugonjwa wa kisukari na ugonjwa wa figo.
  4. Uvutaji wa sigara.
  5. Cholesterol ya juu ya damu.
  6. Unene kupita kiasi.

DALILI ZA KUFELI KWA FIGO KWA MGONJWA WA KISUKARI:

Katika hatua za mwanzo za ugonjwa wa figo uliosababishwa na kisukari mara nyingi dalili huwa hazionekani, lakini katika hatua za baadae mgonjwa anaweza kuwa na dalili kama vile:

  • Shinikizo la juu la damu.
  • Kuvimba kwa miguu, vifundoni, mikono au macho.
  • Mkojo wenye povu
  • Kuchanganyikiwa au ugumu wa kufikiri
  • Upungufu wa pumzi
  • Kupoteza hamu ya kula
  • Uchovu na udhaifu
  • Kichefuchefu na kutapika

MATIBABU YA KUFELI KWA FIGO KWA MGONJWA WA KISUKARI:

Kufeli au kushindwa kwa figo ni hatua ya mwisho ya ugonjwa wa figo na matibabu huwa ni pamoja na:

  • Dialysis ya figo: Tiba hii huondoa taka na maji ya ziada kutoka kwenye damu. Hemodialysis huchuja damu nje ya mwili kwa kutumia mashine ambayo inafanya kazi ya figo. Kwa hemodialysis, unaweza kutembelea kituo cha dialysis takribani mara tatu kwa wiki. Au unaweza kufanyiwa dialysis nyumbani na mwangalizi aliyefunzwa. Na kila kipindi huchukua takribani masaa matatu hadi matano.

  • Upandikizaji wa figo: wakati mwingine figo inapofeli au kushindwa, matibabu bora huwa ni upandikizaji wa figo au upandikizaji wa figo-kongosho. Ambapo mgonjwa hufanyiwa uchunguzi ili kujua kama anaweza kufanyiwa upasuaji.

  • Matibabu au usimamizi wa dalili: Kwa mgonjwa ambaye hataki kufanyiwa dialysis au kupandikiza figo, huweza kufanyiwa matibabu ya zile dalili anazoziona ili kumuweka vizuri kwa miezi michache atakayoishi.

VITU VYA KUFANYA KUPUNGUZA HATARI YA KUFELI KWA FIGO KWA MGONJWA WA KISUKARI:

  • Kukutana na timu yake ya afya mara kwa mara,

  • Kupata matibabu ya ugonjwa wa kisukari

  • Kudhibiti shinikizo la damu

  • Kuwa na uzito wa wastani kiafya

  • Kuacha kuvuta sigara

Subscribe to Medikea newsletter

Sign up here to receive our wellness and health newsletters filled with actionable advice, from certified doctors, expert-vetted content, product recs, and more — delivered directly to your inbox.