JE, NI KWELI UNAHITAJI KUNYWA VIDONGE VYA VITAMINI NA “SUPPLEMENTS” KILA SIKU?

Dr Kuduishe Kisowile

Dr Kuduishe Kisowile

JE, NI KWELI UNAHITAJI KUNYWA VIDONGE VYA VITAMINI NA “SUPPLEMENTS” KILA SIKU?

Ukweli ni kwamba wengi hawahitaji kutumia supplements kabisa kwani kiasi cha vitamini na madini anayopata kutoka katika lishe kinakidhi mahitaji ya mwili. Tofauti na virutubisho kama wanga, protini na mafuta ambavyo vinahitajika katika mwili kwa kiwango kikubwa (macronutrients), vitamini na madini huhitajika kwa kiwango kidogo (micronutrients)

Je, napataje virutubishi hivi kwa njia ya asili?

Virutubisho hivi hupatikana kwa kula mlo kamili na vinginevyo kama vile vitamini D hupatikana pia kwa kupata jua la asubuhi.

Vyakula ambavyo vinakupatia vitamini na madini ni kama vile;

Vitamini A - hii husaidia kuona, ngozi kunawiri na ukuaji. Hupatikana kwenye karoti, mayai, viazi vitamu, samaki Vitamin B - hupatikana kwenye nafaka, vyakula jamii ya karanga, samaki, nyama

  • B1 huboresha mfumo wa neva

  • B2 husaidia uponyaji wa tishu

  • B3 husaidia mwili kuwa na nguvu

  • B9 maarufu kama Folic Acid husaidia ukuaji na afya ya mwanamke wakati wa ujauzito

  • Vitamin D : husaidia unyonywaji wa madini ya Calcium katika mwili na kupelekea meno na mifupa yenye nguvu. Hupatikana kwenye mwanga wa Jua, mayai, maini ya ng’ombe, samaki

  • Vitamin C : husaidia kulinda mwili dhidi ya magonjwa, kuponya vidonda, na unyonyaji wa madini ya Calcium na Maidni chuma kutoka kwenye chakula. Hupatikana kwenye machungwa, broccoli, pilipili, nyanya, matunda aina ya berries

  • Calcium : husaidia ukuaji wa meno na mifupa na kupatikana kwenye maziwa, karanga

  • Madini Chuma : husaidia katika utengenezaji wa seli hai nyekundu za damu na hupatikana kwenye mbogamboga za kijani, nyama nyekundu, karanga

Je, ni wakati gani vidonge vya vitamini na supplements hutumika kwa usahihi?

Vidonge hivi hutumika kwa usahihi pale mtu anaposhauriwa na mtoa huduma za afya kutumia dawa hizi ambapo huandikiwa kulingana na hali yake ya afya.

Mfano; wanawake wajawazito na wanaojiandaa kupata ujauzito wanatakiwa kutumia vidonge vya Folic Acid kwa afya yao na watoto wao kuepusha watoto kuzaliwa na mgongo wazi. Pia, watu wanaoishi maeneo ya baridi sana yasiyopata jua kwa muda mrefu hushauriwa kutumia vidonge vya Vitamin D kwasababu Jua ni kiini kikubwa cha virutubisho hivi.

Vile vile, wagonjwa wenye magonjwa ya mfumo wa damu, mifupa nk hushauriwa kutumia virutubisho hivi kulingana na matokeo ya vipimo vyao vya kiafya.

Tofauti na imani ya wengi, vitamini hazikingi dhidi ya saratani, magonjwa ya moyo au magonjwa ya mfumo wa chakula.

Je, kuna hatari yoyote ukitumia supplements bila ushauri wa mtoa huduma za afya?

Ndio. Dozi kubwa ya virutubishi hivi hubadili namna mifumo mbalimbali ya mwili hufanya kazi. KUMBUKA, Vitamini na madini ni virutubishi vinavyohitajika katika mwili kwa kiwango kidogo (micronutrients). Hivyo basi, matumizi makubwa ya virutubishi hivi hepelekea matatizo mbalimbali ya kiafya.

Mfano; matumizi makubwa ya Vitamini C hubadili uwezo wa mwili kunyonya madini ya Copper kutoka kwenye chakula ambayo ni muhimu katika mwili. Matumizi makubwa ya madini ya Fosforasi (Phosphorus) huzuia unyonywaji wa madini ya Calcium mwilini hivyo kupelekea tumbo kuuma na kuharisha.

Matumizi ya Vitamin D kwa muda mrefu huongeza uwepo wa madini ya Calcium mwilini kupita kiasi hivyo kupelekea mifupa kuwa dhaifu na mawe katika mfumo wa mkojo.

Angalizo:

Licha ya matumizi ya virutubishi kuwa maarufu miaka ya hivi karibuni, epuka kutumia bila kufanya vipimo vya afya na kupewa ushauri wa mtoa huduma za afya kwa ku chat au video call kupitia Medikea App ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea kutokana na kutumia virutubishi kuliko kiwango kinachohitajika mwilini. Kula lishe bora yenye mlo kamili na hutahitaji virutubishi hivi kama afya yako ni bora.