Tiba ya degedege kwa watoto

undefined

Elizabeth Adolph

Tiba ya degedege kwa watoto

Inaweza kuwa vigumu kutambua degedege kwa mtoto kwa sababu si zote hufanana. Mtoto mmoja anaweza kupata degedege mbili tofauti katika vipindi viwili tofauti na hii hutegemeana na sehemu gani ya ubongo imehusika au ukubwa wa degedege husika kwenye ubongo kwa kipindi hicho.

Dalili zifwatazo zita rahisisha wazazi na walezi kutambua degedege nyumbani:

  • Kukakamaa kwa mikono, miguu au mwili mzima. Hii inaweza kuhusisha upande mmoja au hata kiungo kimoja.
  • Kutetemeka kwa mikono, miguu, mwili au kichwa.
  • Kupoteza fahamu
  • Ukosefu wa ufahamu au/na kutoweza kuitikia (wakati mwingine unapomuita mtoto wako na asisikie na kuitika kana kwamba hayupo)
  • Kuzungusha macho.
  • Mabadiliko ya kupumua.
  • Kutokwa na povu mdomoni.
  • Kutoa mkojo na kinyesi bila hiari wakati wa degedege.

Ni muhimu kwa wazazi/walezi kuwa watulivu anapodhani mtoto anapata degedege ili waweze kueleza kwa kina kile kilichotokea kwa wahudumu wa afya na katika baadhi ya matukio kuchukua video wakati wa tukio kutasaidia utoaji wa matibabu sahihi .

Degedege linaweza kudumu kwa sekunde au dakika chache lakini wakati mwingine hudumu zaidi. Degedege kwa zaidi ya dakika 5 kwa watoto ni vyema uende kwenye chumba cha dharura.

Je unafikiri mtoto wako ana degedege?

Ndio,Mwanangu amepatwa na degedege.

Nifanye nini?

  1. TULIA
  2. Hesabu degedege inatumia dakika ngapi mpaka kuacha
  3. Muinamishe alale ubavu wa kushoto ili kumsaidia kupumua.
  4. Mlaze kichwa chake juu ya mto au kitu laini.
  5. Ondoa chochote chenye madhara (kigumu, chenye ncha kali, cha moto) karibu yake.
  6. Ondoa chochote kinachombana.
  7. Ondoa nguo za ziada na nzito kwa watoto wenye homa wakati wa degedege.

Je uende kituo cha afya au umuite daktari wako????? Ikiwa unaweza kuonana/kuzungumza na daktari au daktari wa familia, unapaswa kupiga simu hata kama imetokea kwa muda mfupi, ni muhimu kupata maoni ya wataalam .

Nenda kituo cha afya kama:

  • Hii ni degedege ya kwanza kwa mtoto wako au huna uhakika na kilichotokea.
  • Degedege ilichukua zaidi ya dakika tano.
  • Mtoto wako hajaamka au anaonekana mgonjwa sana baada ya degedege kumalizika.
  • Mtoto wako tayari alikuwa mgonjwa kabla ya degedege.
  • Ikiwa mtoto wako amepatwa na degedege zaidi ya moja.

USIFANYE VIFWATAVYO:

  • Usiweke kijiko au kitu chochote kinywani mwa mtoto wako. Usihofu,mtoto wako hatameza ulimi wakati wa degedege.
  • Usijaribu kusimamisha mitetemeko ya viungo vya mtoto wako
  • Usimsaidie mtoto kupumua kwa kumpulizia hewa mdomoni . Mtoto anatarajiwa kuanza tena kupumua kawaida baada ya degedege. Ikiwa mtoto ameshindwa kurudia hali yake ya kupumua baada ya degedege, nenda kituo cha afya.
  • Usimpe mtoto wako maji au chakula hadi apate ahueni kamili na anaweza kufata maelekezo.
  • Usimweke mtoto wako kwenye beseni la kuogea au beseni la maji ili kupunguza homa yake wakati wa degedege.

KUMBUKA

Degedege inaweza kuwa ngumu kutambua na daima inatisha kwa wazazi kushuhudia, kutoa msaada kwa mtoto na kufanya maamuzi sahihi. Madaktari wa Medikea wanaweza kukusaidia kupitia mchakato huo taratibu na kwa usahihi pamoja mkifanya maamuzi ya kufanya huduma ya kwanza nyumbani au kwenda kwenye kituo cha afya.

Subscribe to Medikea newsletter

Sign up here to receive our wellness and health newsletters filled with actionable advice, from certified doctors, expert-vetted content, product recs, and more — delivered directly to your inbox.