“Tayari Nina Watoto Lakini Sipati Tena Mimba” - Ugumba wa aina ya pili

Medikea Clinic

Medikea Clinic

“Tayari Nina Watoto Lakini Sipati Tena Mimba” - Ugumba wa aina ya pili

Kutokuweza kupata mtoto ni tatizo ambalo linazikumba familia nyingi, na mara nyingi wanawake hulaumiwa kwa kuonekana kama wao ndio chanzo cha tatizo hili. Japo ukweli ni kwamba tatizo linaweza kusababishwa na wote yaani mwanaume na mwanamke.

Hali ya mwanamke kutokuweza kushika ujauzito na mwanaume kutokuweza kusababisha ujauzito huitwa ugumba. Kwa kawaida ugumba upo wa aina mbili:

  1. Ugumba wa kimsingi (Primary infertility): ambapo mtu ambaye hajawahi kushika mimba au kupata mtoto hapo awali anapata shida ya kushika mimba.
  2. Ugumba wa pili (Secondary infertility): ambapo mtu ameshawahi kushika mimba moja au zaidi na kuzaa watoto, lakini anatatizika au anashindwa kushika mimba tena.

Kulingana na takwimu za afya tatizo la ugumba wa pili huwaathiri mamilioni ya wazazi. Wazazi wengi wamekuwa wakijiuliza “kwanini sipati tena mimba wakati tayari nina watoto?”

Sababu za ugumba wa pili (Secondary infertility):

  • Matatizo ya mbegu za kiume: uzalishwaji hafifu wa mbegu za kiume, idadi ndogo ya manii na mbegu ambazo hazisogei vizuri husababisha ugumu wa mbegu kusonga na kurutubisha yai.
  • Kuziba au kuharibika kwa mirija ya uzazi: uharibifu wa mirija ya uzazi husababisha yai kushindwa kusafiri hadi kwenye mfuko wa uzazi hivyo kusababisha mbegu ya kiume kutokutana na yai.
  • Ovary kushindwa kutoa mayai ya uzazi.
  • Kovu kutokana na endometriosis: ambapo tishu zinazofanana na tishu zinazozunguka ndani ya uterasi hukua nje ya uterasi kwenye viungo vingine vya pelvisi.
  • Matatizo yanayohusiana na ujauzito uliopita au upasuaji
  • Magonjwa ya zinaa (STIs): magonjwa ya zinaa kama vile klamidia huweza kusababisha maambukizi katika mfumo wa uzazi (PID) ambayo huweza kuharibu na kutia makovu kwenye mirija ya uzazi hivyo kusababisha ugumu wa yai kusafiri hadi kwenye tumbo la uzazi.
  • Tatizo la umri: uzazi hupungua kulingana na umri unavyoongezeka. Hivyo wanawake wenye umri zaidi ya miaka 35 huweza kusumbuliwa na tatizo la kushika mimba.
  • Tatizo la uzito: uzito kupita kiasi au uzito mdogo sana huweza kuathiri mchakato wa kutolewa kwa yai hivyo kupelekea mwanamke kushindwa kushika mimba.

Jinsi ya kutibu tatizo la ugumba wa pili.

Kuna aina kuu tatu za matibabu ya uzazi ambayo ni kama ifuatavyo:

  1. Dawa: dawa za kawaida za uzazi zinajumuisha:
    • Clomifene
    • Tamoxifen
    • Metformin
    • Gonadotrophins

Dawa hizi husaidia kuchochea ovulation na kuhimiza utolewaji wa yai. Na zinatolewa na daktari bingwa wa uzazi kwa kuzingatia sababu ya ugumba, na uwepo wa magonjwa mengine ambayo yanaweza kuathiriwa na matumizi ya dawa hizi.

  1. Upasuaji
  • Upasuaji wa mirija ya uzazi
  • Upasuaji wa kurekebisha kizuizi cha epididymal na upasuaji wa kurejesha manii.
  1. Usaidizi wa utungaji mimba: hii huhusisha:

    • Upandikizaji wa mimba kwa utiaji wa mbegu ndani ya uterasi (IUI)
    • Utungishaji wa kiinitete kilichorutubishwa maabara (IVF)

Chaguzi za matibabu ya ugumba zinategemea sababu za ugumba hivyo ni vyema kwenda kupima na kufahamu ugumba ulionao umesababishwa na nini ili kujua ni njia gani ya matibabu unapaswa kupatiwa.

Onana na daktari mbobezi wa ugumba na uzazi (Fertility Specialist)

Kwa majibu ya maswali uliyonayo, ushauri na matibabu ya tatizo la ugumba wa pili ni muhimu kuonana na daktari mbobezi wa uzazi (Fertility Specialist) kwaajili ya msaada stahiki. Unaweza kuonana na daktari kwa kuweka miadi kwa kupiga simu 0763100093 au kuchat na daktari moja kwa moja kupitia Medikea App iliyopo iphone na android.

Subscribe to Medikea newsletter

Sign up here to receive our wellness and health newsletters filled with actionable advice, from certified doctors, expert-vetted content, product recs, and more — delivered directly to your inbox.